Zaidi
ya waandishi wa habari 150 pamoja na wanaharakati wa kutetea haki za
binadamu nchini Burundi, hii leo wameandamana kushinikiza kuachiwa
huru kwa Bob Rugurika mkurugenzi wa kituo cha redio ya RPA
anayeshikiliwa na polisi kwa tuhuma za kuhusika na mauaji ya watawa
watatu raia wa Italia.
Bob
Rugurika mkurugenzi wa kituo cha redio cha RPA alikamatwa kati kati
ya mwezi January mwaka huu saa chache baada ya kituo chake kurusha
mahojiano ya mtu mmoja aliyedai kuwa ni miongoni mwa watu waliohusika
na mauaji ya watawa hao.
Waandamanaji
hao walikusanyika nje ya majengo ya mahakama kuu mjini Bujumbura,
Burundi walikaidi amri ya meya wa jiji aliyewataka wasifanye
maandamano hayo, lakini katika hatua ya kushangaza polisi waliwaacha
waandamanaji hao wakusanyike.
Patrick
Nduwimana mmoja wa waandishi wa habari na mwanachama wa muungano wa
chama cha waandishi wa habari nchini humo, amesema kuwa lengo la
maandamano yao ni kuendelea kudai haki na kushinikiza kuachiwa kwa
Rugurika.
Kukamatwa
kwa mkurugenzi wa kituo hiki kumeendelea kuzusha hofu ya kiusalama
hasa kwa waandishi wa habari na wanaharakati ambao wameendelea
kukamatwa na vyombo vya dola nchini humo kwa tuhuma mbalimbali, hali
ambayo wachambuzi wa mambo wanaona kuwa ni kutaka kuminya uhuru wa
watu kutoa maoni yao wakati huu nchi hiyo ikijiandaa kufanya uchaguzi
wake mkuu.
Aucun commentaire:
Enregistrer un commentaire