Pages

jeudi 18 décembre 2014

BURUNDI, TUME HURU YA UCHAGUZI KULIKONI?

Tume ya Uchaguzi nchini Burundi CENI imekiri dhahiri shahiri kuwepo kwa kasoro zilizojitokeza wakati wa zoezi la kuorodhesha raia kwenye daftari la wapiga kura na kusisitIza kwamba ukiukwaji huo wa taratibu hautokani na uamuzi wa dhati wa Tume hiyo.

Mapema juma hili, vyama vya upinzani nchini humo vimeiomba tume hiyo kujiuzulu ambapo vyama 18 vimeituhumu Tume hiyo kuandika majina ya wapigakura hewa kusaidia chama tawala katika uchaguzi mkuu mwaka 2015.

Vyama hivyo 18 vya upinzani nchini humo vinatishia kuendesha maandamano iwapo madai yao hayatopatiwa jawabu. Vyama hivyo vinaiomba tume ya uchaguzi Ceni pawepo na mazungumzo kuhusu matokeo ya zoezi la kuorodhesha raia wataopiga kura hapo mwakani na pia tume ya uchaguzi Ceni ijiuzulu kwa kuwa si huru.

Kumekuwa na hofu ya kutokea mvutano wa kisiasa nchini Burundi kutokana na hali hii ambayo tume ya Uchaguzi imeendelea kupuuzia madai ya wansiasa wa upinzani, jambo ambalo linaweza kukwamisha mchakato mzima wa uchaguzi kama ilivyoshuhudiwa katika chaguzi zilizopita.

Mbali na ukimya wa wa tume huru ambayo licha ya kukiri kuwepo na dosari imeendelea kusisitiza kwamba kasoro zilizojitokeza zinaweza kurekebishwa, rais wa nchi hiyo Pierre Nkurunziza pia alitakiwa kuingilia kati kuhusu swala hili ili kuhakikisha mchakato wa uchaguzi unashirikisha pande zote, ili baadae ataeangukia pua kwenye uchaguzi akose sababu.

Upinzani wao unaona kuwa kukaa kimya kwa viongozi wa chama tawala ni kutokana na jambo hili kukinufaisha.

Lakini pia Umoja wa Mataifa, Umoja wa Ulaya, mashirika mbalimbali ya kimataifa yameendelea kukaa kimya kutokana na tuhuma hizi za uwepo wa udanganyifu katika zoezi hili la kuwaorodhesha wananchi katika dafatari la wapiga kura.

Kama kweli tume huru yenyewe inakiri uwepo wa kasoro nyingi tu katika zoezi hilo, kwanini madai ya upinzani yasifanyiwe kazi? Mwenyekiti wa tume hiyo CENI Pierre Claver Ndayicariye alisikika akisema kwamba chaguzi zilizopita kulikuwepo na dosari kama hizo, lakini zilirekebishwa, hivi hali ilivyokuwa kipindi hicho ndivyo ilivyo kwa sasa?

Wachambuzi wa siasa wanajiuliza wapo wapi watetezi wa Burundi? Wanasubiri moto uwake ili waje kuuzima wakati kuna uwezekano mkubwa wa kuuzima kabisa usiwake?

Kwa vyovyote vile hakuna ataefaidi iwapo vurugu zitatokea ikiwa chanzo itakuwa na swala hili ambalo baadhi wanalichukulia kuwa la kawaida wakati wengine walichukulia kuwa la msingi.

Tusubiri tuone.

Aucun commentaire:

Enregistrer un commentaire

KINACHOFANYWA NA RAIS NKURUNZIZA KWA SASA NDIO ULE MCHEZO WA NDANI?

Mkanganyiko umeendelea kushuhudiwa katika chama tawala nchini Burundi cha CNDD-FDD, chama ambacho hapo awali kilileta matumaini ya kuwau...